Girls Leadership
Faraja ya Usichana
Faraja ya Usichana
Usichana na Ukuaji
Usichana
Maelezo Juu ya Usichana
ASIKUDANGANYE mtu rafiki yangu, utoto una raha zake, ndiyo maana mara kadhaa unasikia watu wanasema wanatamani kurudi utoto. Kwanza ni kuhusu huduma, hakuna bughudha na fikiria pale baba au mama anapokufuata shuleni kukuchukua ili kukurudisha nyumbani. Au pale unaporejea kutoka shule na kukuta mama amekwisha aandaa msosi, unajichana halafu unaenda kucheza, kweli ni raha tu. Kudeka kama kazi, huku umekunja mashavu kama umenyimwa hela ya kununua pipi!
Lakini miaka inasonga mbele na mambo yanabadilika na hata lile jina 'mtoto', taratibu linaanza kupotea na hapo unaonekana umekua. Kweli unafikia wakati unalazimika kuuaga utoto, hakuna ujanja kwa sababu kama unataka kuendelea kubaki mtoto sasa utakuwa unang'ang'ania tu. Basi tuachane na hayo kwa kuwa sasa mwenzio nimekua wacha nikupe stori za kikubwa, maana tayari nimeshaondoka kwenye huo utoto.

Turudi kule darasani, shoga, hamu yangu yote ya kuwa kama Sara iliniisha siku hiyo. Akiwa amekaa ametulia tuli, mara ghafla ukelele mmoja wa kushtua ulitoka kwa mmoja wetu akisema, 'Sara! Sara! Vipi! Damu!' Hali hiyo ilinitoa kwenye mawazo yangu ya kuhakikisha nafanya vizuri zoezi la hisabati, nikalazimika kuinua macho kutazama kuwa kulikoni Sara, loh! Alikuwa na doa nyuma ya sketi yake.

Sikuelewa, Sara kimemsibu nini, niliporudi nyumbani nilimsimulia dada yangu mkubwa, yeye akanieleza: Sara amevunja ungo, hii ni dalili ya kukua/kubalehe. Nami nikamuuliza dada anieleze mabadiliko nitakayoona mwilini kama dalili za kukaribia kuvunja ungo, walau nijiandae mapema kabisa, jambo hili nisingependa linikute bila maandalizi yoyote
Mabadiliko ya mwili yanayotokea
Maelezo Juu ya Mabadiliko ya Mwili Yanayotokea
Matiti
- Hukua, yanavimba na kuuma kidogo. Mara nyingine moja huwa dogo kidogo kuliko jingine.
Kwapa, Uke
- Huota nywele makwapani na kuzunguka uke. Wingi wa nywele ni tofauti kwa kila msichana, wengine ni chache wengine ni nyingi
Uso (Ngozi)
- Uso hupendeza zaidi, ngozi huwa na mafuta mengi yanaweza kusababisha chunusi kwa wasichana wengine. Hali ya chunusi inaweza ikasumbua hadi kwenye miaka ishirini hivi, halafu ikatoweka.
Nyonga
- Hupanuka, ndiyo sababu yule rafiki yangu Sara alikuwa na kishepu cha kimama, kilichowasumbua wavulana. Mabadiliko haya hutokea ghafla kwa kipindi kifupi kabla ya kuvunja ungo
Urefu
- Urefu huongezeka na uzito pia huongezeka. Wasichana kimaumbile hurefuka na kukua haraka kuliko wavulana tunaolingana nao umri kwenye miaka ya 15 hadi 17. Wavulana wanakuwa na kutupita miaka ya 17 hadi 19.
Tezi za jasho
- Jasho huzidi kutoka kuliko awali na kiharufu cha jasho kinaanza. Hii ni kawaida, cha msingi ni kuzingatia usafi.
Sauti
- Hubadilika kuwa nyororo au kukaza kidogo. Si wote na sauti nyororo hii ni tofauti ya maumbile tu.
Hatimaye...
- Wasichana huvunja ungo kati ya miaka 9 hadi 15 na kipindi hiki chote mwili unajiandaa kwa mabadiliko ya kuwa mtu mzima. Damu huanza kutoka ukeni kila mwezi kwa siku 3-7, inategemea na kila msichana. Kama tulivyoona katika yale mabadiliko yanatokea mwilini. Msichana anapofikia hapa ana uwezo wa kupata mimba.
MIMI NA MWILI WANGU ULIVYO: KABLA NA BAADA YA KUBALEHE


Mzunguko wangu wa Mwezi
Maelezo Juu ya Mzunguko wangu wa Mwezi
Neno mzunguko humaanisha vitu/matukio yanayojirudia-rudia ki mduara. Hapa nina maana ya mwanzo wa hedhi katika mwezi mmoja mpaka inapoanza tena mwezi unaofuata.
Tuchukue mifano hii:

Mzunguko huu kwa wanawake walio wengi ni wa siku 28, unahesabu siku ya kwanza uliyoanza hedhi mwezi huu hadi siku moja kabla ya kuanza hedhi mwezi unaofuata. Wachache wana mzunguko wa siku 21 na wengine wa siku 35. Hii ni aina tofauti ya maumbile wala si ugonjwa. Hata hivyo ili kupata wastani kamili na wa uhakika wa mzunguko wako, unatengeneza kikalenda chako cha siri utakachoweza kurekodi vizuri siku za hedhi za kila mwezi kwa miezi sita (6).Utahesabu kila mwezi mzunguko wake, utajumlisha mizunguko ya miezi yote sita (6) na kuigawa kwa sita (6). Kwa mfano:
- Januari siku 26, Februari siku 28, Machi siku 31, Aprili siku 33, Mei siku 29, Juni siku 28.
- Jumla siku 175 ÷ miezi 6 = siku 29
- Kwa hiyo mzunguko wa uhakika ni siku 29
Vile vile tukichukulia alama za barabarani:

- NYEKUNDU- Daima huashiria hatari
- KIJANI- Ni rangi ya usalama
- NJANO- Huweka tayari rangi ya maandalizi
Mfano wa mzunguko wa mwezi:

Nyekundu:
Hizi ni siku ambazo yai limeshakua, na mji wa mimba umeanza kujengeka ili kukaribisha mimba. Yai husafiri kutoka kwenye kokwa hadi kwenye mji wa mimba kupitia kwenye mirija ya kupitishia mayai. Iwapo litakutana na kuungana na mbegu ya kiume, mimba itatungwa, kisha husafiri kukaa kwenye mji wa mimba
Ishara ya mwili:
- Maji maji yenye kuteleza hutoka na kukufanya ujisikie kama umelowa. Maji maji haya ni kama ute unaovutika mithili ya yai bichi au mlenda.
Kijani:
Siku hizi huitwa siku salama, pengine zilipata jina hili kwa sababu huwezi kushika mimba kwenye siku hizi. Huwa ni baada ya hedhi ambapo yai halijapevuka kwenye kokwa.Baada ya siku hatari, uke huwa mkavu na hizi pia huwa ni siku salama kwani baada ya siku kadhaa yai husinyaa na litatoka na damu ya hedhi.
Njano:
Njano iliyo karibu na nyekundu inaashiria uwezekanao wa yai kuwa tayari kurutubishwa. Njano iliyo karibu na hedhi, ni kipindi ambacho mwili upo katika maandalizi, kiuno na mgongo unaweza kuuma, chunusi hutokea, kichwa kuuma.
Usafi
Usafi ni Mazoea
Mojawapo ya sifa kubwa za mwanamke ni usafi, ni muhimu tuelewe kuwa usafi ni mazoea unayojijengea. Kipindi hiki tuzingatie usafi, viharufu vya ajabu-ajabu vitatuumbua.
Jasho:
Jasho kali au kikwapa ni kutokana na kemikali zilizoko mwilini zinazobadili mfumo mzima wa via vya uzazi. Humo mwilini, vitu vipo kazini kama kiwanda.
- Uoge walau mara moja kwa siku lakini ni bora ikawa mara mbili hasa siku za hedhi au angalau nawa sehemu zako za siri walau mara mbili kwa kutwa.
- Nyoa nywele za kwapani mara kwa mara na kusafisha vizuri na sabuni wakati unapooga. Tumia “deodarant' mafuta ya kukausha jasho na kuondoa harufu kwapani.
- Yanapatikana kwa wingi kwenye maduka mbalimbali hata yale ya mtaani kwako.
- Ogea sabuni ya magadi inakata jasho na harufu kwapani zinapatikana kwa wingi kwenye maduka mbalimbali hasa yale ya magereza
PEDI/ KITAMBAA (SODO)/ PAMBA:
Hivi vitu hatupaswi kuviweka hovyo hovyo hasa tukiwa shuleni, kama mnavyojua wavulana hupenda sana kututania hasa kama watabahatika kuviona na pia si vizuri ili kulinda hadhi na heshima ya mwanamke.
- Damu ya mwezi ikutanapo na hewa hubadilika harufu na kunuka kama kitu kilichooza , hivyo basi, badilisha pedi/kitambaa(sodo)/ pamba kila baada ya saa nne (4) kupita ukizingatia hedhi yako na wingi wake. Kama unatumia kitambaa (sodo) kifue hadi kitakate, kitoke doa la damu. Kama unatumia pamba au pedi usitupe kwenye choo cha kuvuta, huweza kusababisha choo kuziba.
- Usitupe nje jalalani, maana mbwa na paka huweza kuviburuzia kwa watu. Unaweza kuchimbia chini au kuchoma moto.
- Hakikisha nguo zako za ndani ni safi kwa kubadili mara mbili au tatu kwa siku kwa uhakika zaidi.
- Tembea na pedi/ kitambaa/ pamba ukaribiapo siku zako ili kuepuka fedheha ya kuanza hedhi na kuchafuka hadharani.
Usafi, usafi, usafi ni mazoea unayoweza kuyajenga iwapo utajipenda,nawa sehemu zako za siri kila unapobadilisha pedi/ pamba/ kitambaa chako. Vile vile usiache kunawa vizuri mikono yako.
Njia Panda
WASICHANA wengi katika kipindi chetu cha ukuaji hasa miaka michache baada ya kuvunja ungo, hatuna utaratibu maalumu wa mzunguko wa hedhi, mwezi huu inaweza ikawepo na mwezi ujao isiwepo. Mara kwa mara, mzunguko hubadili siku zake kiasi kwamba huwezi kujua siku zipi yai linarutubishwa na siku zipi unakaribia kuanza tena hedhi. Hali hii si ugonjwa bali ni hali ya kawaida, via vya uzazi huwa havijakomaa sawasawa. Cha msingi, ni kuwa makini na mwangalifu bila kuiwekea asilimia 100 kalenda yako. Mimi nikikaribia hedhi nasononeka sana kwa sababu ya maumivu makali ya tumbo.
Maumivu hayo nayapunguza kwa kufanya yafuatayo:
- Kunywa maji moto kwa wingi siku mbili kabla ya kuanza hedhi.
- Kufanya mazoezi ya viungo kuwezesha mvutano wa misuli katika tumbo la uzazi kutokuwa mkubwa
- Wachache hunywa dawa na husema zinawasaidia kupunguza maumivu ambazo ni Panadol na Buscopan ingawa si vyema kujenga mazoea ya kutumia dawa kila mara
Pia...
1. Ninamfahamu msichana mmoja aliyekuwa akitoka damu ya hedhi hata wiki mbili mfululizo, hili ni tatizo la homoni huwa zinazidiana mwilini na ni vizuri kwenda mapema kwa daktari wa magonjwa ya wanawake kwa msaada wa kitaalamu
2. Miezi mingine inapita bila kuwa na hedhi, usiogope, usiingiwe na hofu na hali hiyo kwa kuwa husababishwa na:
- Mabadiliko ya ghafla ya hali ya hewa.
- Kama uliugua sana kwa muda mrefu, au kwa maumivu makali sana.
- Mwanzoni mwa kuvunja ungo, mzunguko huwa hauko sawa mpaka baada ya mwaka hata zaidi.
- Habari zilizo kushtua hasa za huzuni.
3. Wasichana wengine wanafikia miaka 18 bila kuvunja ungo. Hawa ni muhimu kumuona daktari wa magonjwa ya wanawake mapema.
YOTE HAYA NI KENDA LA KUMI NAJIVUNIA KUWA MWANAMKE
Msichana na Jamii
Ukuaji wangu na Jamii
Maelezo ya ukuaji wangu Kijamii
Kijamii
- Nilionekana ghafla mtu mzima na kutoeleweka pale nilipoendelea na michezo ya utotoni.
- Majukumu yangu nyumbani yalibadilika pia kwani sasa nilianza hata kuwapikia chakula tofauti na ilivyokuwa hapo awali.
- Niliachiwa wadogo zangu kuwaangalia, kuwafulia, kuwapeleka shule

- Bibi yangu kila mara alinikanya kuhusu nguo zangu tena alisema “Umekua sasa, Si vizuri kuvaa nguo fupi na zinazoonyesha maumbile yako”

- Nilifokewa kuhusu kuongea mara kwa mara na kucheza na wavulana

Katika kukua nikatambua haya:
- Hakuna mtu asiyejua kuwa wewe bado ni mtoto, jitahidi kuweka ratiba ya kila kitu ili hata muda wako wa kucheza ubaki palepale, shoga ndio ukubwa huo. Ujue, kucheza ni mazoezi ambayo ni muhimu kwa afya yako
- Mama au bibi anafurahia sana kumuona bintiye amekuwa mtu mzima, naomba uwaelewe, hivyo basi hupenda kukuandaa kuwa mwanamke au mama bora. Ni vyema akina mama na akina bibi wawe wazi kwa wasichana. Ukweli ni kwamba nyumba nzuri huwa na msingi mzuri pengine hata wewe ukijaliwa kuwa mama utafanya hivyo-hivyo kwa bintiyo
Kisaikolojia
- Nilikuwa njia panda, utoto naupenda na ukubwa nautaka, kote kulinivuta na sikuelewa nikimbilie upande upi hasa.
- Hata kama nimekuwa mkubwa sikujua nifanyeje, kwani wakubwa wakoje? Lakini mbona mimi ni mdogo?
Mpenzi wangu hata wewe yanakukuta haya hata kama ni mfumo tofauti kidogo, haya basi tusaidiane:
Hata yule anayepandishwa cheo akiwa na miaka 40 anakuwa na hali hiyo hiyo ya kuogopa kuvuka hatua nyingine kutokana na mazoea aliyojenga sehemu aliyopo. Utakutana na hii hali mara nyingi maishani, uizoee na kuwa jasiri.
- Hakuna tabia ya mtu iliyo rahisi kuiga. Kitu kizuri ingawa kigumu maishani ni kuwa wewe mwenyewe na uhalisia wako, inapendeza na ni bora zaidi kama ukihakikisha hauigi mambo ya mtu fulani. Unatakiwa ujikubali, ujipende na pia ujivunie kuwa wewe. Uwe mdadisi wa kuelewa mambo na kujifunza yaliyo ya manufaa kwako.
Uhusiano na wengine
- Mh, Adam siku hizi anavutia sana yaani ni mtanashati ile mbaya halafu mcheshi na tulimchagua kuwa kiranja darasani kutokana na jinsi alivyo. Akisimama mbele ya darasa mikono yangu inatoa jasho.
- Nawaonea aibu wavulana, wakikaa kwenye kundi njiani, niko radhi nibadilishe njia kuwaepuka

- Basi bwana, siku moja Adam alitumwa na mwalimu kuniita. Akaja kunichukua kwa kunishika mkono, siwezi kukueleza nilivyojisikia mpaka kesho sikumbuki alichonieleza mwalimu siku hiyo manake mawazo yote yalikuwa mkononi
Rafiki yangu huu ni wakati ambao hisia juu ya jinsi ya kiume huanza kujitokeza kwa nguvu sana.
- Huo, mpenzi wangu, ni mvuto wa kawaida si tamaa. Usiruhusu ukutawale.
- Usiwaogope wavulana, wachukulie kama marafiki wa jinsia moja hii itakusaidia kujenga kujiamini ndani yako.
- Tafuta unachopendelea (hobby), michezo au masomo utakayoweza kuzingatia ili kupoteza hizo fikra.
- Ongea na mama au dada juu ya hali hiyo kwa sababu wanakupenda na hawawezi kukupotosha kamwe.
- Siyo kila kitu utakachosikia ni cha kweli kuhusu uhusiano na afya ya uzazi, tukiwa shuleni kila mtu ana tabia zake; kuigaiga mambo, hicho si kitu kizuri, jifunze kuiamini dhamira yako.
Ukuaji wangu Kiuchumi
Maelezo ya ukuaji wangu Kiuchumu
Kiuchumi:
- Ukigeuka kushoto Rehema anaringa na saa yake mpya, kanunuliwa na mpenzi wake. Jana alikuja na mkebe (kompasi) mpya kabisa alisema kanunuliwa pia.
- Kuna anko kila nikitoka shule namkuta kwenye kona ndani ya gari ananisubiri. Siku ya kwanza alivyoniita alinipa 10,000/= nilifurahi kwa sababu nilihitaji kununua vitu vingi lakini baadaye nikaogopa.

Maisha hayana njia ya mkato, tamaa ikiendekezwa tutayakatisha maisha yetu mazuri tena kwa mwisho mbaya.
- Kila kitu kina wakati wake, pesa zipo na zinakungoja iwapo utakuwa na bidii shuleni na kuweza kutumia akili yako utazipata.
- Ukizoea kupewa hela za bure hautaweza kukaa na kujifunza kuzitafuta mwenyewe kwa kufanya kazi. Na kama hizo za bure zitaacha kuja kwa njia hiyo basi utataabika mno na hata kuingia kwenye vishawishi ambavyo ni hatari zaidi kwa afya na maisha yako kwa ujumla.
- Mtu anayetoa hela ili umpende maana yake hakuthamini na amekuchukulia kama ng'ombe kwenye mnada, dau la mnunuzi linapanda muuzaji anapozidi kukataa.
- Usiuze utu wako kwa vilifti, viji-chipsi kuku, simu, ice cream, urembo na kadhalika. Jipende na kuwa jasiri hayo ni majaribu tu ya nafsi unayoweza kuyaepuka
Msichana na Mahusiano
Afya ya Uzazi
Maana ya afya ya Uzazi
Afya ya uzazi ni ipi?
Katika pilika zangu nilipita sehemu kadhaa na kukutana na watu mbalimbali. Miongoni mwa hao watu nilipenda kufahamu wanaelewa nini juu ya afya ya uzazi, nao walinijibu ifuatavyo:
- Ni afya ya kupanga uzazi wa watoto kwa maana nyingine uzazi wa mpango katika familia.
- Ni ile inayomhusu mama mjamzito mpaka anapofikia kipindi cha kujifungua mtoto wake.
- Afya ya wanandoa hasa inayohusu tendo la kujamiiana ili kupata watoto.
Niligundua watu hawa wako gizani lakini mimi pia ilikuwa hivyo hivyo na kilichonipa utata ni neno hili la uzazi
Nini maana ya afya ya uzazi?
- Ni afya inayohusu maungo ya uzazi yaani via vinavyohusika katika mtiririko wa kupata mtoto kuanzia kujamiiana hadi mimba inapotungwa katika mfuko wa uzazi.
- Uzazi ni uwezo wa mbegu ya kike kurutubishwa na ya kiume ili kutungwa mimba.
- Afya ya uzazi inahusu jinsia zote za kiume na za kike kwa sababu wanaume nao wana via vya uzazi
- Afya ya uzazi inabidi kutiliwa maanani na kulindwa katika mzunguuko wote wa maisha: toka utotoni hadi uzeeni.
Ngono katika umri wangu
NAAMINI kuwa kila uendapo umesikia na kuambiwa juu ya matokeo ya kufanya ngono katika umri mdogo. Naona kama nisirudie, lakini nafikiri ni vyema kama nitakueleza yafuatayo ambayo mimi pia nilielezwa na yakanisaidia:
- Uamuzi wa kufanya ngono ni wako wala mtu mwingine hana haki ya kukushawishi au kukulazimisha, nasema hivi kwa sababu asilimia 95% hufanya tendo hili si kwa hiari yao.
- Misingi imara ya dini yako itakupa nguvu na uwezo wa kukabili vishawishi,kwa mimi mkristo,imani yangu ni nguzo yangu
- Starehe ya muda mfupi inaweza kukuletea majuto ya muda mrefu katika maisha yako yote.
- Uelewe kuwa wewe ni mtu muhimu sana “spesho”hapa duniani na mwili wako ni kielelezo cha undani wako hivyo basi inakupasa uulinde mwili wako.
- Ndoto zako hazitofanikiwa bila jitihada, nguvu zako na uwezo wako. Jifunze kujipenda na kujithamini na sio kutimiza matakwa ya mtu mwingine.
- Hata kama wote walio karibu yako au unaowafahamu wanafanya tendo hili, jivunie kuwa tofauti
Umri sahihi wa kufanya ngono ni upi?
Kuna imani za dini,mila na desturi ama maazimio binafsi yanapelekea watu kufanya ngono wakiwa kwenye ndoa, hiyo ni sahihi na bora. Pia, wengine, labda kutokana na sababu zao nyingi,muhimu na ambazo sio muhimu, wanataka kufanya ngono kabla ya ndoa.
Uamuzi wa kufanya ngono uzingatie yafuatayo:
- Mipaka yako ya dini na maadili yenu,kuepuka kutumbukia dhambini
- Ndoto zako na mipango yako inayohitaji kutekelezwa, mara nyingi katika umri wa wanafunzi ni mapema mno
- Utu wako, heshima yako na kulinda nafsi yako.
- Uhusiano madhubuti na kijana anayekupenda ambaye pengine mtaoana na haitakufanya ujutie.
- Jitahidi kusubiri upate mchumba anayefaa. Mbele tutaona mchumba anayefaa ni yupi ili usiruke ruke huku na kule kama kuku asiyekuwa na makazi maalum Uwe umekuwa kifikra, kimsimamo na mwenye hesabu na mipangilio madhubuti kwa maisha yako.
Unyanyasaji wa kijinsia
Maelezo juu ya Ngono ya kulazimishwa
Ngono ya kulazimisha: ubakaji
Kwanza kabisa hebu tuwekane sawa, unajua wengi kati yetu mimi nikiwa mmojawapo sikuelewa kuwa ngono ya kulazimisha ndiyo ubakaji. Ukweli ni kuwa mtu mzima anaweza kumshawishi msichana mdogo wafanye ngono bila hata kumnasa kibao. Msichana huyo akiwa chini ya miaka 18 basi huyo mtu aliyemfanyia kitendo hicho atahukumiwa kwa mujibu wa sheria ya ubakaji.
Tendo la kubaka
Ni kumlazimisha mtu kufanya nae mapenzi kinyume na ridhaa yake hali inayoweza kuleta majeraha makubwa kimwili na kisaikolojia kwa mtu aliyebakwa kwa muda mrefu sana
Hatua ya kwanza kama umebakwa
- Ni uamuzi wako kutoa taarifa, kuripoti polisi au usiripoti. Lakini ni vema kuripoti tukio hilo polisi ama kwa mtu yeyote unayemwamini anayeweza kutoa msaada. Iwapo utaamua kutoa ripoti polisi basi nenda kwenye kituo cha karibu na tukio lilipotokea na pia nenda hospitali ya karibu kama umeumia sana na wao watakutibu na baadaye nenda polisi.
Hatua za kuelewa iwapo umeamua kwenda polisi
- Usijisafishe wala kujifuta kwa sababu utapoteza ushahidi ambao utahitajika mahakamani.
- Jiandae kwenda mahakamani iwapo polisi watamshika aliyekubaka
- Daktari atachunguza kwa nia ya kutafuta ushahidi utakaosaidia kesi yako ili mbakaji aweze kuhukumiwa
Nilisikitika pale nilipoongea na msichana mmoja ambaye alienda kuripoti kituoni kuwa amebakwa. Polisi wale wakaanza kuongelea kwa sifa umbile lake tena ngoja ninukuu walivyosema “du! Zinga la figa, jamaa uzalendo ulimshinda ha ha ha………! Hii ilinidhihirishia jinsi wanaume walio wengi walivyo na mtazamo wa ubaguzi wa kijinsia.
- Iwapo umeamua kutotoa ripoti polisi ni lazima utibiwe kama kuna madhara yoyote yaliyotokana na kitendo hicho. Pia kumbuka, unahitaji dawa ya kukinga maambukizo ya UKIMWI ama magonjwa mengine ya ngono.
- Usikae kimya,itakuumiza, ongea na mama dada, bibi au mtu yeyote unayemwamini ili hilo donge lisikae tena ndani yako.
Sipendi kufikiria hili suala lakini yanatokea ...
Mimba itokanayo na kubakwa
Kuzaa mtoto wa mbakaji ni wazo la kwanza litakalokujia kichwani kwako hata hivyo ni mtoto wako pia. Mimba hiyo unaweza kuamua kuzaa lakini ni muhimu baada tu ya kitendo hiki uende hospitali ili pia uweze kufahamu hali kama hii. Ukishafahamu kama huitaki, unaweza kupewa njia ya dharura ya kuzuia mimba
Magonjwa ...
- Muhimu ni kuanza dawa za kutibu magonjwa ya ngono mapema iwezekanavyo na ndio maana nasisitiza umuhimu wa kwenda hospitali kitendo hiki kitokeapo. Pigo kubwa ni kama amekuambukiza virusi vya UKIMWI ni ngumu hata kwa kufikiria tu lakini katika maisha kuna kuendelea mbele. Pata ushauri nasaha kuhusu virusi vya UKIMWI na kutokukata tamaa.
Vidonge vya dharua vya kuzuia mimba vipo katika vituo vya afya hapa nchini. Iwapo utabakwa, ili uweze kuzuia mimba, nenda katika kituo chochote cha afya na uripoti suala hilo. Inatakiwa umuone mtoa huduma ya uzazi wa mpango ambaye atakupa ushauri pamoja na huduma. Mimba inaweza kuepushwa kwa usalama na kwa ufanisi hadi siku tatu au saa 72 baada ya kubakwa. Jinsi utakavyowahi kumeza vidonge vya dharura vya kuzuia mimba, kuna uwezekano mkubwa wa kuepuka mimba
Mtoto nizae Mtoto ?
Maelezo juu ya Mtoto Kuzaa Mtoto
Nitakuwa mgeni wa nani mie...!
Katika akiba yangu nilikuwa na vijihela kidogo bila kusita nikaenda hospitali moja niliyoelekezwa na shoga yangu kwa nia ya kuyasitisha maisha ya huyo kiumbe aliyeko tumboni. Nilikuwa nimetajiwa mpaka dokta, nilimuulizia na nikaelekezwa ofisini kwake, Haukupita muda tukajikuta tukipangiana bei kama vile ukiwa unanunua nguo halafu unaomba upunguziwe bei
Baada ya makubaliano aliniuliza kama nimekula nikamwambia hapana hata hivyo nilipenda kujua maana ya hilo swali akaniambia atanichoma sindano ya usingizi inayoleta kichefuchefu hivyo basi haitakiwi niwe nimekula kwa sababu matapishi yanaweza yakapita njia ya hewa na kusababisha kifo.
Nikavaa manguo ili nipelekwe chumba cha operesheni. Licha ya kupewa dawa ya usingizi huko kwenye chumba cha operesheni nikaanza kusikia wanachokifanya kwa mwanangu.
Sitanii wala sidanganyi, wanakwangua kama nazi inavyokunwa kwenye mbuzi. Nilihisi kizunguzungu, nikalala. Eh! Nimesahau kuwaambia hizo sindano zinachomwa pale palenukeni halafu wanaingiza kama bomba ili wapanue njia. Usikie tu, inauma, Baada ya pale, walikuwa wameniwekea gozi kama pamba ndani kwa ajili ya kunyonya damu. Ilipofika jioni nikatoa gozi lakini damu ikaendelea kutoka kwa fujo ikiwa mabonge mabonge na tumbo lilianza kuuma nashindwa hata kueleza. Damu iliendelea kutoka kama bomba lililofunguliwa. Niliumwa nikahisi nakufa. Nilienda hospitali nyingine na kufikia hatua hii hata nyumbani walijua. Niliingizwa tena chumba cha operasheni nikasafishwa upya, maumivu yalipungua taratibu na tumbo likaacha kuuma. Sijajua kama nina uwezo wa kubeba mimba tena kwa sababu yaliyonikuta hata rafiki yangu wa kiume aliniacha.Yaliyonifika nisingependa yamfike msichana mwenzangu, jamani!
Njia za Kuzuia Mimba
Maelezo juu ya Njia mbali mbali za Kuzuia Mimba
Zipo katika makundi haya mawili
- Njia za kisasa
- Njia za asili
NJIA ZA ASILI
1.Kutokufanya ngono kabisa
Hii ni njia madhubuti na yenye uhakika kwa asilimia 100.
2. Kufanya ngono siku salama za mwezi:

Msichana anachunguza mabadiliko ya ute wa ukeni kila siku kwa kutumia vidole vyake, yeye na mwenzi wake wanaweza kuzuia mimba kwa kuepuka kujamiiana katika siku za kupevuka yai. Njia hii haina uhakika wa moja kwa moja na wakati mwingine ni vigumu kufuatilia ratiba ya kupevuka kwa yai hasa inapotokea mabadiliko ya ghafla yasiyotarajiwa.
NJIA ZA KISASA
1. Njia za vizuizi
- Kondom ya kiume,Huu ni mpira laini ambao huvishwa kwenye uume uliosimama kabla ya kujamiiana. Mpira huu huzuia shahawa kuingia ukeni ili kusababisha mimba kutunga. Kondom mpya itumike kwa kila mshindo mmoja na kutupwa kwa usalama.

- Kondom ya kike,Huu ni mpira laini ambao unaingizwa ukeni na kuushikisha kwenye mlango wa uke. Mpira mpya hutumika kwa kila tendo la kujamiiana kisha kutupwa kwa usalama

2. Dawa zenye vichocheo
- Vidonge vya uzazi wa mpango,Vidonge hivi vina dawa maalum inayoweza kuzuia mimba.Vina maelekezo yake kwenye pakiti na ni njia ya muda, ni salama na ya kuaminika. Hivi ni vidonge ambavyo humezwa na mwanamke kila siku ili kuzuia mimba. Hupatikana katika pakiti ya vidonge 28 na 35. Vidonge hivi pia husaidia kurekebisha matatizo ya hedhi.

- Sindano,Hii ni njia ya uzazi wa mpango inatolewa kwa kuchoma sindano kwenye msuli wa bega au takoni. Utumiaji wa njia ya sindano huzuia mimba kwa kipindi cha miezi mitatu

- Vipandikizi,Hii ni dawa ya kuzuia mimba ambayo imo ndani ya mrija wa plastiki, wengine huviita vijiti. Mwanamke huwekewa vipandikizi (na mtaalam) chini ya ngozi, kwenye sehemu ya ndani ya mkono. Vipo vipandikizi vya aina mbili: vyenye vijiti sita na vyenye kijiti kimoja

3. Njia za muda mrefu na njia za kudumu
- Kitanzi (copper T), Hiki ni kiplastiki kidogo kilichozungushiwa na shaba kwa sehemu chache ambacho kinawekwa na mtalamu kwenye mji wa mimba (mfuko wa kizazi) ili kuzuia mimba isitunge. Kitanzi kina uwezo wa kuzuia mimba kwa kipindi cha miaka 8 hadi 10. Kitanzi kinaweza kutolewa wakati wowote mwanamke anapohitaji kupata mimba.

- Kufunga kizazi kwa mwanamke, Hii ni njia nyepesi ya operesheni ndogo ambayo hufanyiwa mwanamke aliyeridhika na idadi ya watoto aliowapata. Kwa kawaida operesheni hii hufanyika kwa muda usiozidi dakika ishirini . Baada ya saa 2 hadi 6 kupita, mteja anaweza kwenda nyumbani. Kufunga kizazi kwa mwanamke hakuathiri hamu yake ya kujamiiana, wala mzunguuko wa hedhi.

- Kufunga kizazi kwa mwanaume, Hii ni njia nyepesi ya operesheni ndogo ambayo hufanyiwa kwa mwanaume aliyeridhika na idadi ya watoto aliowapata. Kwa kawaida operesheni hii hufanyika kwa muda usiozidi dakika kumi na tano. Baada ya saa 2 hadi 4 kupita, mteja anaweza kwenda nyumbani. Kufunga kizazi kwa mwanaume hakuathiri hamu yake ya kujamiiana, wala nguvu za kiume.

MAMBO YA KUKUMBUKA
- Uzazi wa mpango hauingilii haki ya mtu binafsi au wenzi katika kuamua idadi na wakati wa kupata watoto
- Unahitaji kuwa na taarifa kamili na sahihi ili uweze kuchagua njia ya uzazi wa mpango: Mtoa huduma atakusaidia kufanya maamuzi sahihi.
- Kondom ndiyo njia pekee inayokinga mimba, magonjwa ya ngono na UKIMWI
- Kondom hupatikana madukani, lakini pia zinapatikana bila ya malipo kwenye vituo vya huduma za afya.
Maelezo juu ya dondoo mbali mbali na mambo muhimu ya kukumbuka
DONDOO ZA UZAZI WA MPANGO, VVU/UKIMWI
- Watu walioambukizwa VVU wanaweza kutumia njia za uzazi wa mpango
- Uzazi wa mpango huwapunguzia adha za ujauzito wanawake walioambukizwa VVU
- Vijana wanapoahirisha kuanza ngono huwapunguzia uwezekano wa kuambukizwa magonjwa ya ngono/VVU na kuepuka mimba katika umri mdogo. Hivyo wanaweza kufikia malengo yao ya kimaisha
UKWELI HUTUWEKA HURU
Ni dhahiri kwamba kuna njia mbali mbali za kuzuia mamba lakini tuelewe tu ya kwamba mimba iliyokwishatunga,imeshatunga.Iwe dakika moja baadae,saa moja baadae hata siku moja baadae,maisha ya binadamu huyo tayari yameshaanza.Kwa maana nyingine,huzuii mimba bali unaua kiumbe cha Mungu. Nimesema haya,lakini mwishoni wa siku uamuzi unabaki kuwa wa kwako na ndio maana nimejitahidi kuweka bayana hizo njia zote.
TOFAUTI YA NGONO NA MAPENZI
Ngono ni tendo la kujamiiana baina ya mwanaume na mwanamke kwa nia ya kuridhishana kimwili.
Mapenzi ni hisia kali za mvuto baina ya mtu na mtu. Upendo wa dhati ambapo hutaki kumwona mpenzi wako anaumia, na huu ni upendo unaojali na kuheshimu
- Tuelewe ngono sio lazima iwe na mapenzi, tunaweza kufanya ngono na watu bila kuwa na mapenzi nao.
- Ngono ni sehemu ndogo tu ya uhusiano wa kimapenzi na muda mwingi katika mapenzi hutumika kujenga mazoea.
- Wasichana tuna hulka ya kuchanganya ngono tukidhani ni mapenzi, wavulana wanaelewa ngono ni ngono na mapenzi ni mapenzi matokeo yake tunaumia.
Shoga usifuatenmkumbo wa kufanya ngono kwa kujionyesha ya kwamba wewe unafuata “fashion”. Heshimu mwili wako, usikubali kufanya ngono holela. Mwanaume anayetaka kukuoa ataheshimu msimamo wako wa kutotaka kufanya ngono kabla ya wakati muafaka
Unawezaje kujikinga na UKIMWI?
Njia kuu ambazo zinaweza kukusaidia usipate UKIMWI
- Subiri; usifanye ngono kabisa mpaka wakati muafaka utakapofika: kuolewa au kuwa na mwenzi wa kudumu (Kwa lugha ya kiingereza: Abstinence”A”)
- Kuwa na mwenzi mmoja mwaminifu ambaye hajaambukizwa Virusi Vya UKIMWI (Kwa lugha ya kiingereza: Be faithful ”B”)
- Tumia Kondom kila mara na kwa usahihi: Mshauri mwenzi wako kutumia Kondom ya kiume au tumia mwenyewe kondom ya kike (Use Condom ”C”)
Nimechagua “A”
Muda unavyozidi kwenda mimi na mpenzi wangu tunazidi kufurahi pamoja na mpango wa kuondoka unazidi kupotea. Giza linazidi kuingia, kwenye redio unasikika muziki laini unaobembeleza. Nahisi niko karibu sana na mpenzi wangu. Kila kitu ni sawa, hisia zangu kwa kweli ni kali. Nahisi mpenzi wangu yuko tayari kufanya mapenzi na kwa namna moja mimi pia niko tayari.
Nifanyeje?
- Wengi wetu tumepitia hali hii na wewe pia, mwenzangu, lazima katika kukua upitie hali hii inayokufanya ukabiliwe na wakati mgumu wa kufanya uamuzi. Mara nyingi unajikuta katikati ya mahaba mazito bila kufahamu nini hasa unataka,ukifikiria kama ufanye au usifanye.
La kufanya :
- Ni vizuri kuongea mkiwa hampo kwenye mahaba mazito tayari kuhusu uamuzi wako wa kutofanya ngono. Chagua wakati ambao mmetulia na mkiongea mtaelewana na upange kabisa utakachokiongea kabla mazungumzo hayajaanza
- Kama umeamua kutofanya ngono basi usiwe kama kinyonga unabadilika badilika. Maneno yako na matendo yako yaendane. Wote wawili mnapaswa mkubaliane mipaka yenu. Shoga tawala hisia, usiruhusu hisia ikutawale!
Ni vigumu iwapo:
- Mtakaa peke yenu chumbani na mpenzi wako.
- Mtakutana sehemu za giza au vichochoroni mkiwa wawili na mna uhakika hakuna anayewaona.
- Mnakunywa pombe mpaka mnalewa kiasi unashindwa kufanya mamuzi sahihi..
- Mnaangalia mikanda ya video ya ngono, picha, karata au magazeti ya ngono pamoja au peke yako.
- Ukikaa na rafiki zako mazungumzo ni kufanya mapenzi, ukikaa na mpenzi wako pia mazungumzo ni hayo hayo. Inakuhamasisha zaidi kufanya ngono.
Ni rahisi iwapo
- Mtatafuta hobi ambayo wote mnapendelea iwe michezo, masomo au sanaa.
- Kujichanganya na rafiki zenu au watu wengine na sio kukaa peke yenu kila mara kama vile mko kwenye fungate(honeymoon)
- Kuepuka kukaa chumbani au vichochoroni peke yenu ili msijihamasishe kufanya ngono..
- Mimi naamini msichana ndiye mtu wa kwanza kufanya maamuzi juu ya mwili wake, juu ya mipango na ndoto zake. Maamuzi ambayo mwishoni yanalenga kumjenga na sio kumdidimiza. Fanya uamuzi ambao hautajutia siku zijazo, mwezi mmoja au mwaka mmoja baadaye

Kwa nini usubiri?
- Nilivyokuwa shule nilielezwa kuwa tendo la ndoa ni kwa wanandoa na ndio maana limeitwa tendo la ndoa. Hata wakati nakua, nilisisitizwa jambo hilo, hasa kwa sababu za kidini na imani zetu na hii ndiyo sababu yenye nguvu zaidi. Pale sababu hii inapovunjwa tunajihisi kujisaliti wenyewe na Mungu wetu,hata kuchanganyikiwa kwa kuhisi umepoteza muelekeo.
- Maazimio binafsi yasiyohusishwa na dini wala mila hufanya watu wengine kusubiri,unaweza kuwa mmoja kati ya wa watu hawa.
- Sababu ya iliyo wazi kwa wengi kuliko zote ni ile ya kuzuia mimba na magonjwa ya ngono hasa UKIMWI.
- Wasichana tuna tabia moja ya kihisia tena yenye kutuumiza. Tuingiapo katika hali ya mapenzi na mtu inakuwa sio tu kimwili bali tunajitoa zaidi kihisia, kama kuna asilimia basi kimwili ni 40% tu ama chini ya hapo na asilimia nyingi huenda kwenye hisia. Tunatekwa haswa. Kwa hiyo ni muhimu kujilinda, kwani furaha au huzuni inapotawala kutokana na mapenzi, vitu vingine vyote ikiwemo shule, familia n.k vinatoweka akilini.
Tuwe marafiki
- Usidanganyike rafiki yangu, uhusiano mzuri ni ule uliojengwa juu ya msingi imara. Msingi huo ni urafiki. Mapenzi ni kuzoeana, kuelewana na kuheshimiana. Ukichemka mwanzoni maana yake umechemsha moja kwa moja.
- Kuharakisha mapenzi badala ya kujenga urafiki inaweza kuumiza uhusiano wenu na hasa hisia zako.
Shikilia uamuzi wako
- Tatizo linakuja hapa, umeshaamua hutaki kufanya mapenzi kwa sasa. Mpenzi wako unampenda ndio umefika, utawezaje kushikilia uamuzi wako bila kuumiza hisia zake.
- Mwisho wa siku,haya ni maisha yako,mkimbilie Mungu wako mwenye upendo unaodumu, naye atakuongoza njia ya kupita.Unaweza kuwa bora,unaweza kuwa jasiri,unaweza kuwa chochote unachotaka kuwa iwapo utaamini.

Listening to this topic